Sunday, October 9, 2016

Maeneo ya Jiji la Dar es Salaam Yanayoongoza Kwa Uporaji

Unashauriwa kukaa chonjo iwe usiku au mchana. Bisibisi ndiyo silaha maarufu, na wizi wa bodaboda hutumika zaidi kuliza watu.

Yafuatayo ni maeneo hatari jijini Dar es Salaam ambayo haijalishi umepita muda gani ili mradi una simu, fedha, vito vya dhahabu, ‘silver’ au mali nyingine. Wenyewe wakikuona kama hujaambulia kibao cha kukupumbaza, utatishiwa na silaha ili utoe ulicho nacho na wengine hutumia madawa ya kulevya kabisa.

Watu hao bila kujali ni asubuhi, mchana au jioni, wamekuwa wakipora na wakati mwingine wamekua wakipora bila haya ya kujali kama kuna wapita njia wengine eneo husika, huendelea na shughuli zao badala ya kukimbia kama ilivyozoeleka.

Kundi kubwa ambalo limetajwa kulizwa na waporaji hapa mjini ni wanawake kutokana na udhaifu walio nao na mara nyingi vibaka huamini pochi wanazobeba hazikosi chochote. Vibaka hao wamekuwa wakitumia viwembe, visu, bisibisi, kamba au kumpiga mhusika kwa lengo la kumtisha atoe alicho nacho.

Maeneo ambayo yametajwa kukithiri vitendo vya uporaji katika wilaya ya Ilala ni Majumba Sita njia panda ya Segerea, Tazara, Msimbazi Centre, ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Coco, Daraja la Salendar, barabara ya Ocean, Majani ya Chai na Lugoda.

Kwa upande wa Kinondoni ni Tanganyika Parkers kuelekea ufukwe wa bahari Kawe, Makuburi ya Kinondoni, Mkwajuni, kituo cha daladala cha Mwenge, Tandale kwa Mtogole, Mwananyamala A na Mwananyamala kwa Mama Zakaria, maarufu kama mahakama za simu.

Katika wilaya ya Temeke, wananchi wameyataja maeneo ambayo ukipita lazima ukabwe na kuporwa ulicho nacho kuwa ni mataa ya Chang’ombe, BP Kurasini, Temeke Maguruwe, pori la kiwanda cha Bia ambako kuna maficho ya wahalifu na Mbagala Kiburugwa ambako ni maarufu kama mbwa mwitu. Lipo pia eneo la kati ya Mbagala Kizuiani na Zakhem. 

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta