Mwandishi wetu alimshuhudia Babu Seya akiwa Muhimbili chini ya ulinzi wa askari magereza watatu na wafungwa wengine watano katika Jengo la Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) huku akiwa amedhoofu.
Haikuweza kujulikana mara moja ugonjwa uliosababisha Babu Seya ahamishiwe Muhimbili kwa matibabu kwa sababu Jeshi la Magereza lina hospitali yake na mwandishi alipoomba kwa mmoja wa askari magereza ili aweze kumsalimia mwanamuziki huyo, hakupewa ruhusa.
Baadhi ya wananchi waliomshuhudia mwanamuziki huyo akiwa Muhimbili na kuingizwa katika chumba cha daktari namba 112 walisema, anavyoonekana ni dhahiri ni mgonjwa kwa sababu hakuwa mchangamfu kama ilivyo kawaida yake.
“Nguza (Babu Seya) mara nyingi huwa mchangamfu lakini leo amekuwa mnyonge, mwili umepungua na hata ngozi yake siyo ang’avu, bila shaka anaumwa sana,” alisema mwananchi mmoja hospitalini hapo.
Hata hivyo, mara baada ya matibabu, Babu Seya aliingizwa katika gari la magereza na kurudishwa Gereza la Ukonga kuendelea kutumikia kifungo chake.
Dodosadodosa ya mwandishi hospitalini hapo ili kujua kinachomsumbua Babu Seya, haikuambulia chochote kwani daktari mmoja alisema ni mwiko kwao kutaja ugonjwa wa mgonjwa bila ridhaa yake na ni kinyume cha maadili ya kidaktari.
“Umeniuliza anaumwa nini, kwanza mimi siye niliyemtibu lakini hata kama ningejua ugonjwa wa Babu Seya, siwezi kukuambia ni unethical (kinyume cha maadili). Lakini kweli ni mgonjwa na ndiyo maana ameletwa hapa kutibiwa,” alisema daktari huyo aliyekuwa nje ya jengo moja akizungumza na mwanamuziki huyo.
Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, Eddy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanaye Papii Kocha kwa kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti watoto wa Shule ya Msingi Sinza-Mapambano, Dar na kuwafunga kifungo cha maisha jela huku rufaa ya kesi yao ikiwekwa kiporo kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyopo jijini Arusha.
Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii