Wednesday, June 22, 2016

Magufuli Ashusha Nyundo 7, Apasua makampuni ya madini, Mafao hewa na miamala ya simu

Rais John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameendelea na kasi yake ya kutumbua majipu ambapo jana alishusha nyundo kwa majipu mapya 7 yanayotafuna uchumi wa nchi kwa kuiibia Serikali kwa mbinu mbalimbali kupitia miamala ya fedha.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Rais Magufuli alisema kuwa Serikali yake haiwezi kuyavumilia makampuni ya Madini yanayofanya kazi nchini kwa kuendelea kuieleza Serikali kuwa yanapata hasara miaka yote huku yakiendelea na shughuli zake za uchimbaji madini.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa kama Makampuni hayo yanasema yanapata hasara kila mwaka ni bora yaondoke nchini.

Hivyo ni visingizio tu, ni bora tubaki na madini yetu miaka 1,000 watachimba watakaokuja sisi tukiwa tumeoza,” alisema.

Wanadai wanapata hasara wakati wana akaunti sehemu nyingine,” aliongeza Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia alieleza kuwa tayari amebaini kuwepo kwa malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 7 yasiyo ya halali (hewa) kwa wastaafu 2,800 kupitia Benki ya NMB. Katika hilo alieza kuwa tayari ameshatoa maagizo watu hao warejeshe fedha hizo.

Pia, Rais Magufuli amelikamua jipu udanganyifu kwenye miamala ya simu. Alisema amebaini kuwa makampuni ya simu yamefanya miamala yenye thamani ya shilingi trilioni  5.5 ambayo haikukatwa kodi, mwezi Machi mwaka huu.

Aliwataka TCRA kushirikiana na BOT  kuhakikisha wanalishughulikia suala hilo na kurejesha fedha za serikali kupitia kodi.

Rais Magufuli pia aliyanyooshea kidole maduka ya kubadilishia fedha za kigeni akiitaka BOT kuyasimamia kwa ukaribu ili yasiwe kichochoro cha kupitishia fedha za dawa za kulevya ama fedha ambazo zinavushwa kinyamela.

Kadhalika, Rais Magufuli aliwataka BOT kuhakikisha kile walichomueleza kuwa wamewezesha kushuka kwa mfumuko wa bei kwa kutoka asilimia hadi asilimia 5.2 kionekane kwa uhalisia ka wananchi na sio kuishia kwenye maandishi.

Je, [kushuka huko]kumefika kwa wananchi au kumeishia kwenye makaratasi tu? Je, bidhaa za miaka ya 90 na sasa ni sawa?” Rais Magufuli anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemuagiza Gavana wa BOT, Profesa Benno Ndulu kuifuta Benki ya Twiga Bancorp kwakuwa imekuwa ikijiendesha kihasara huku ikivunja sheria.

Alimtaka Gavana Ndulu kuzichukulia hatua Benki zote zenya muelekeo huo hata kama ni za Serikali.

Unakwenda Benki unakuta kuna negative (hasi) bilioni 18, mimi nasema katika utawala wangu sitabembeleza Benki isiyofanya vizuri hata kama ni ya Serikali. Kuna Benki moja inapambwa na CCM lakini….” Rais Magufuli alisikika japo hakuitaja Benki hiyo.

Rais Magufuli pia aliitaka BOT kuhakikisha Benki zinaweza kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kunusurua taasisi na wananchi wanaokopa katika benki hizo.

Naye Gavana Ndulu alimhakikishia Rais Magufuli kuwa wanaunga mkono juhudi zake na kumkabidhi mfano wa hundi ya shilingi bilioni 4 ambayo watatoa kwa serikali kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari nchini. Gavana ndulu alisema kuwa fedha hizo zimepatikana kutokana na kubana matumizi.

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta