Monday, May 23, 2016

Video: Kauli ya Mkuu wa Mkoa Makonda Kwa Benki Zilizokua Zikilipa Mishahara Watumishi hewa

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 21 kwa benki zilizokuwa zikitumika kuweka mishahara ya watumishi hewa, kurejesha fedha hizo serikalini ; au kubainisha waliokuwa wakitumia akaunti hizo, kuchukua fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makonda alisema benki ndio pekee wanaoweza kusaidia mkoa, kutambua wahusika waliokuwa wanatumia akaunti hizo pamoja na wale waliokuwa wanachukua fedha hizo.

Alisema watu hao wasipopatikana, inamaanisha fedha bado zipo katika benki hizo, hivyo zinapaswa kuzirudisha serikalini zifanye maendeleo kwa wananchi. 

“Tayari tumeshaziandikia benki hizo barua na kuwapatia majina na akaunti na kuwataka kutuwasilishia majina ya wahusika, waliohusika na akaunti hizo ili kusaidia kutambua mtandao mzima wa wahusika wa suala la watumishi hewa ambao wameigharimu serikali,” alisema Makonda.

Alitaja benki hizo pamoja na fedha wanazodai kuwa ni benki ya NMB ambayo inadaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili, CRDB zaidi ya milioni 400, NBC zaidi ya milioni 141, DCB milioni 85, Standard Chartered zaidi ya Sh milioni mbili na Community Benki zaidi ya milioni 100.

“Hakuna mtu anayeweza kutumia akaunti ya mtu bila kufuata taratibu za kibenki, hata kama mtu amefariki kuna taratibu za kufuata ndipo apate akaunti, naamini benki hizi zitasaidia kuwatambua wahusika wote,” alisisitiza.

Aidha, alizitaka benki hizo kufunga huduma za akaunti hizo ;na zisifanye malipo yoyote mpaka fedha hizo zitakapopatikana. 

Mpaka sasa, Mkoa wa Dar es Salaam umebainika kuwa na watumishi hewa 283, ambao wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 3.6 ambazo zilitumika kuwalipa mishahara.

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta