Thursday, May 12, 2016

Spika Job Ndugai Awagomea Wabunge Waliotaka Utaratibu wa Kusaini Mara Mbili Kwa Vidole Ufutwe

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amejibu mwongozo ulioibuliwa na wabunge bungeni wa kutaka utaratibu wa kusaini kwa kutumia kidole mara mbili kwa siku uondolewe, kwa kusisitiza kuwa utaratibu huo hautabadilishwa.

Majibu ya mwongozo huo aliyatoa bungeni Dodoma jana wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), aliyemtaka Spika autolee majibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Konde Khatib Said Haji hivi karibuni wa kutaka utaratibu huo ufutwe.

“Mheshimiwa Spika inaonesha kuna dalili ya Bunge lako kutojibu miongozo inayoulizwa hapa bungeni. Hivi karibuni tuliuliza juu ya namna ya kusaini kwa kutumia madole sijui kidole lakini mpaka leo hatujapatiwa majibu,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Ndugai alijibu kwa kifupi kuwa utaratibu wa kusaini wabunge ni mara mbili kwa siku na wanatakiwa wakandamize kidole chao hadi taa ya kijani iwake ndipo watakuwa wamesajiliwa rasmi.

“Nataka nitoe ufafanuzi, nasikia kuna malalamiko juu ya utaratibu wa kusaini, maagizo ni hivi, unaposaini pale kandamiza kidole chako hadi taa ya kijani iwake, utakuwa tayari umesajiliwa si kugusa tu. Ule mfumo unaitwa press and hold,” alisema Spika na kufunga mjadala wa suala hilo.

Hivi karibuni, Mbunge Haji, aliomba mwongozo na kuitaka ofisi ya Bunge iwaondolee mara moja utaratibu wa kusaini kwa kutumia vidole mara mbili kwa siku kwa kuwa wao si wanafunzi.

Katika mwongozo wake, alisema kitendo cha kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku ni kero kwa wabunge na uonevu kwa kuwa hata Bunge hilo limekuwa likitumia muda wa mapumziko wa wabunge kwa kazi za Bunge.

“...tatizo langu ni kitendo cha wabunge kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku asubuhi na jioni, wakati mwingine tunatoka hapa saa saba, wabunge tunashughulikia mambo mpaka saa 12, mbunge anatumia muda wake wa mapumziko na ule wa kuhudhuria kikao cha jioni,”alisema.

Alisema inasikitisha kuona mbunge anatolewa kwenye kazi za kujenga taifa ili aje tu asaini kwa kidole tena mara ya pili. 

Alisema jambo hilo linawatatiza wabunge kwa kuwa wanajiona kama wanachukuliwa kama wanafunzi kwa kufuatiliwa kwani hata kwenye benki wafanyakazi hawasaini na kufuatiliwa kama ilivyo kwa wabunge hao.

Alifafanua kuwa kabla ya kuomba mwongozo huo, alifanya utafiti kwenye benki mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao nao wana utaratibu kama huo wa Bunge lakini hakuna mahali wanapotakiwa kusaini kwa vidole mara mbili.

Kwa upande wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson wakati akijibu mwongozo huo alisema kutokana na namna wabunge hao walivyopokea suala hilo, pamoja na kwamba kikanuni jambo hilo halikutakiwa kuombewa mwongozo bado litaangaliwa. 

“Hata hivyo nifafanue kuwa kusaini mara mbili lengo lake si kuwafanya wabunge wanafunzi, ila lengo ni kutaka kujua nani wapo humu ndani (bungeni),” alisema Dk Ackson.

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta