Jana, mkurugenzi wa elimu ya mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema ripoti ya Panama Papers ni chachu ya mamlaka hiyo kufanya uchunguzi wa kina na wa kimataifa ili kujua iwapo kuna chembechembe za ukwepaji kodi kwa kampuni hizo za Watanzania.
“Kwa kutumia mbinu tulizonazo, tutafuatilia iwapo kampuni hizo zimekwepa kodi wanayopaswa kulipa hapa nchini,” alisema.
Kayombo alisema watatumia mbinu zote, kama Polisi wa Kimataifa(Interpol) na benki zinazohusika pamoja na kuchunguza miamala iliyofanywa na kampuni hizo kujua iwapo wamekwepa kodi.
“Hatuwezi kuzungumza kwa kina kwa sababu tutaharibu uchunguzi wetu, lakini kwa kifupi tutawa-trace (wafuatilia) wote,” alisema.
Juzi, timu ya Umoja wa Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ), yenye makao makuu Washington, ilitoa orodha ya zaidi ya watu 200,000 wakiwamo Watanzania wenye kampuni nje ya nchi.
Jumla ya Watanzania 45 na kampuni zaidi ya nane zenye uhusiano na Watanzania zimeorodheshwa kwenye ripoti hiyo iliyobatizwa jina la Panama Papers.
Miongoni mwa Watanzania waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa aliyestaafu, Rostam Aziz, ambaye ameeleza kuwa hakuna ubaya kuwa na kampuni iliyosajiliwa kwenye visiwa hivyo.
Mwingine ni Yusuf Manji, mkurugenzi mstaafu wa kampuni ya Quality Group Ltd, ambaye pia ameeleza kuwa hakuna tatizo kumiliki kampuni zilizosajiliwa nje.
Pia yumo mbunge wa Morogoro Mjini na mfanyabiashara anayemiliki vyombo vya habari na usafirishaji, Abdulaziz Mohamed Abood, ambaye aliiambia Mwananchi juzi kuwa hana taarifa za ripoti hiyo ya Panama. Ripoti ya Panama inaeleza kuwa kampuni ya sheria ya Mosack Monseca ilihusika katika kusajili kampuni hizo na mwanzilishi wake akiwa ni Ramon Fonseca.
ICIJ imesema nyaraka zilizovuja na kutumiwa kwenye uchunguzi huo haziwezi kuwekwa bayana kwa kuwa zinahusisha baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa hawakufanya makosa.
Jinsi wanavyokwepa kodi
Akizungumza na Mwananchi jana, Selius Mkwizu wa kampuni inayojihusisha na uchunguzi wa kodi nchini, alisema kampuni zinazofunguliwa nje ya nchi zinafuata unafuu wa kodi katika visiwa hivyo.
Kwa kawaida, visiwa hivyo huzitoza kampuni za nje ya nchi kodi isiyozidi asilimia 5 au chini ya hapo kwa ajili ya kuvutia soko la wawekezaji.
Hivyo, alisema wafanyabiashara wakubwa au wanasiasa hukimbilia na kufungua akaunti na kusajili kampuni kwenye nchi hizo na wakati huo huo hufanya ujanja ili wasikatwe kodi ya kampuni kwenye nchi yao.
Kwa hapa nchini ili kampuni iliyofunguliwa nje ya nchi ifanye kazi kihalali, inatakiwa ilipe asilimia 30 ya kodi ya kampuni au (corporate tax) kutokana na faida ambayo imepata. “Hata hivyo, wafanyabiashara na wanasiasa huhifadhi fedha zao kwenye akaunti za kampuni hizo (nje ya nchi) halafu baadaye huandika ripoti ya uongo inayoonyesha wamepata hasara na hivyo hawakatwi kodi,” alisema.
Kwa kawaida ili kampuni ikatwe kodi, ni lazima iwe imepata faida au wanahisa wamepata gawio kutokana na faida iliyopatikana.
Mkwizu alieleza zaidi kuwa mara nyingi kampuni hizo ni hewa na jina lake hutumika kwenye akaunti kwa ajili ya kuweka fedha tu. Lakini kiuhalisia hazipo wala hazifanyi shughuli yoyote huko.
Namna wanavyocheza na nyaraka
Mwandishi wa ICIJ iliyotoa ripoti ya Panama, Will Fitzgibbon aliiambia Mwananchi kuwa wamiliki wa kampuni hizo huweza kukwepa kulipa kodi kwa kufanya mambo tofauti.
Alisema kwanza wanaweza kutunga uongo kwenye taarifa za fedha za mwaka na kuonyesha kampuni yao iliyo nje ya nchi imefanya matangazo, imefanya ukarabati, imelipa ada ya usimamizi au imefanya huduma za masoko kwa hiyo imepata hasara.
“Kwa maana hiyo basi, kama taarifa ya fedha ya kampuni hiyo itaonyesha kuwa imepata hasara, basi haitakuwa na vigezo vya kukatwa kodi kwa kuwa kodi ya kampuni inatokana na faida,” alisema.
Alisema ICIJ wamegundua kuwa licha ya kampuni hizo kudai kuwa zimepata hasara, wanahisa au bodi ya wadhamini wanaonekana kupata gawio, kujenga nyumba za kifahari au kumiliki mali zenye thamani kubwa kwenye nchi hizo.
Alisema kingine kilichobainika ni wamiliki wa kampuni hizo kuwa na kampuni nyingine ambazo wamiliki wake ni ndugu zao kama vile mpwa, dada au kaka . Hivyo, kampuni hizo hupata zabuni kutoka kampuni mama.
“Ujanja mwingine ni kampuni kuwa na bodi ya wadhamini ambao ni ndugu wa karibu, wanafamilia na kampuni yenye jina moja kufanya kazi nchi zaidi ya moja,” alisema.
Hata hivyo, Fitzgibbon alisema bado nyaraka za Panama zitaendelea kutoa taarifa za namna kampuni hizo zinavyokwepa kodi.
Kanuni za ‘offshore’
Ili kupambana na uhamishaji wa fedha unaohusisha ukwepaji wa kodi, Februari 7, 2014 Tanzania ilitambulisha kanuni mpya ya Kodi ya Mapato inayohusu gharama za kuhamisha fedha (Transfer Pricing Regulations). Kanuni hizi zinawagusa walipa kodi wote walio ndani na nje ya nchi, lakini iwapo tu kampuni itaonekana haijapata hasara.
Kama kampuni imepata hasara, haitakatwa kodi.
Kanuni za gharama za kuhamisha fedha zinaangalia miamala iliyofanywa na watu au kampuni zinazofanya kazi nje.
Kadhalika zinaangalia namna kampuni hizo zinavyohamisha kiasi cha faida au gawiwo la faida kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Hata hivyo, Mkwizu alisema kanuni hii ni dhaifu kwa kuwa ni vigumu kwa nchi kufuatilia na kujua iwapo kampuni iliyofunguliwa kwenye visiwa hivyo imefanya kazi zilizoainishwa kwenye taarifa ya fedha na kama kweli ipo.
BOT wazungumza
Wakati TRA ikijipanga kuchunguza suala hilo, Benki Kuu imesema kutolipa kodi kwa sababu yoyote ile ni uhalifu na lazima ushughulikiwe.
Meneja uhusiano wa Benki Kuu, Zalia Mbeo alisema usajili wa kampuni nje ya nchi unatakiwa kufuata taratibu za nchi husika na za kimataifa. Hata hivyo, alisema lazima utaratibu huo uwe na manufaa kwa muhusika na nchi anayotoka.
“Ndiyo maana tuna Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi na ambao wanarejesha nyumbani fedha nyingi za kigeni kutokana na mapato yao halali,” alisema.
“Tunaamini kwamba ukiukwaji wa taratibu za usajili kwa lengo lolote, likiwamo la kutolipa kodi ni uhalifu kama uhalifu mwingine na unapaswa kushughulikiwa na mamlaka husika,” alisema
Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii