Mzimu wa kuzuia shughuli za Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni uliopachikwa jina la ‘Bunge Live’, umeendelea kumwandama Waziri wa Habari, Nape Nnauye baada ya juzi kupokewa kwa kelele kiasi cha kushindwa kuhutubia wapenzi wa muziki jijini Mwanza.
Nape alitangaza uamuzi wa kusitisha kurusha moja kwa moja baadhi ya shughuli za Bunge, akisema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linashindwa kumudu gharama, lakini wabunge, hasa kutoka vyama vya upinzani wamepinga hatua hiyo wakisema inawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata habari kuhusu chombo chao cha kutunga sheria.
Lakini Serikali imeshikilia msimamo wake, ikitoa sababu tofauti na kwenda mbali zaidi kuzuia vituo binafsi vya televisheni kurusha matangazo, huku TBC1 ikirusha kipindi cha maswali na majibu pekee ikielezwa kuwa huo ni uamuzi uliopitishwa katika Bunge la 10.
Juzi, Nape aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha la Jembeka Festival lililofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, alipokewa na kelele za maneno “Bunge Live” wakati akikaribishwa kuhutubia mamia ya wapenzi wa burudani waliohudhuria tamasha hilo, ambalo lilijumuisha wasanii nyota kama Shaffer Chimere Smith a.k.a Ne-Yo kutoka Marekani na Diamond Platnum.
Baada ya mkurugenzi wa kampuni ya Jembe ni Jembe, Sebastian Ndege kumkaribisha waziri huyo kuzungumza na wananchi hao, Nape alisimama lakini akapokewa kwa kelele.
“Bunge live, Bunge live, Bunge live,” walipiga kelele mashabiki waliohudhuria tamasha hilo.
Kelele za “Bunge Live” zilisababisha Waziri Nape kushindwa kuhutubia na kulazimika kuketi chini na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula alisimama kujaribu kuokoa jahazi, lakini naye akakumbana na kimbunga cha sauti za wananchi walioamua kulitaja jina la mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Ezekia Wenje.
“Wenje, Wenje, Wenje,” wananchi hao waliimba kwa sauti wakati Mabula akijaribu kuwatuliza ili Nape ahutubie.
Akizungumzia tukio hilo, Nape alisema wananchi waliompigia kelele za “Bunge Live” walisukumwa na masuala ya kisiasa, ndiyo maana aliepuka kuendelea kuzungumza ili kutochafua hali ya hewa uwanjani.
“Pale uwanjani tulikwenda kwa ajili ya burudani, sasa baada ya kuona wananchi wanaanza kuleta masuala ya kisiasa nikaona ni busara kuacha kuhutubia. kuepusha shari,” alisema Nape.
Pamoja na Nape, tamasha hilo pia lilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mabula.
Ukiachilia mbali dosari hizo, tamasha hilo lilikonga nyoyo za wapenzi wa sanaa ya muziki waliokesha uwanjani hapo hadi saa 11:00 alfajiri wakiburudishwa na wasanii nguli.
Wasanii wengine waliopata nafasi ya kutumbuiza ni Juma Nature, Ney wa Mitego, Ruby na Fid Q.
Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii