MWENYEKITI wa Mtaa wa Bulale wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Alphonce Nyinzi (48) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika wakati akielekea nyumbani kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 22 mwaka huu majira ya saa 2 usiku.
Msangi amesema kuwa marehemu aliekuwa akifahamika kwa jina maarufu "msukuma" mfanyabiashara na mkazi wa bulale aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na kutokea chini ya kwapa upande wa kulia na watu wawili wasio fahamika pamoja na risasi hiyo kumjeruhi Neema Marangula (23) Mkazi wa Bulale katika Kiganja cha mkono wa kulia.
Amesema kuwa wakati Mwenyekiti huyo akitoka kwenye kikao alichofanya na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mtaa wa Bulale akiongozana na wajumbe wawili alikutana na Neema Marangula akiwa na mume wake ambao walikua wanawafuata marehemu na Balozi kwa ajili ya kuzungumzia mzozo wa ndani ya ndoa yao kwa hiyo walikua wanahitaji kusuluhishwa.
Mwenyekiti huyo (marehemu) na wajumbe wake wawili wakiwa pamoja na Neema pamoja na mumewe wakiwa wanajadili tatizo hilo hapo barabarani mara ghafla wakatokea watu wawili ambao walikua wakipita barabarani na kuwaambia mko chini ya ulinzi na mmoja wao akatoa bunduki na kumpiga risasi mwenyekiti huyo ambaye alianguka chini huku wenzake wakikimbia kujiokoa kutoka eneo hilo lakini pia wale wahalifu wakakimbia na kutokomea gizani vichakani.
Amesema wananchi wa eneo hilo ambapo mwenyekiti aliuawa walijitokeza kwa msaada wa kumsaidia walimchukua na kumkimbiza hospitali kwa matibabu lakini alifariki dunia wakiwa njiani. majeruhi Neema Marangula amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi wa daktari, chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika pamoja na uchunguzi tukio hilo bado unaendelea.
Msangi amewaomba wananchi wenye taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo zitakazo saidia kufanikisha kukamata wahusika wazitoe polisi lakini pia kutoa ushirikiano kwa viongozi wao na kuhakikisha wanatengeneza makazi salama huko wanapoishi na maeneo ya shughuli zao na msako mkali unafanyika na kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa.
Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii