Sunday, May 15, 2016

Jaji Mkuu: Sheria Ya Makosa ya Mtandaoni Haina Lengo la Kuwakandamiza Watanzania


JAJI MKUU wa Tanzania, Mohammed Chande Othman amesema sheria ya mitandao ilipitishwa kwa lengo jema la kulinda watumiaji, wanajamii na usalama wa Taifa la Tanzania.

 

Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Mei 14, 2016) wakati akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa Watanzania waishio Uingereza kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza.

 

Alisema watu watatu kati ya wanne nchini Tanzania wakiwemo watoto, wanamiliki simu za mkononi ambayo ni sawa na watu milioni 35 kati ya milioni 45.

 

Alisema sheria hiyo ilitungwa kwa misingi mitatu moja ikiwa ni kumpa mtumiaji uhuru wa kutoa maoni au taarifa, uhuru ambao alisema unalindwa kikatiba lakini akaonya kuwa kila uhuru unaotolewa pia una mipaka yake kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 30(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Alisema sheria hiyo pia inatoa uhuru wa mtu kuwa na faragha (privacy) na msingi wa tatu ni sheria hiyo kuzingatia matumizi ya mitandao ili kulinda usalama wa nchi.

 

“Sheria hii inakupa uhuru wa kutumia mtandao kumlinda mwanajamii wenzako. Hapa Uingereza nimeongea na mwendesha mashtaka mkuu ambaye aliniambia kuwa asilimia 60 ya makosa yanayofanyika chini ya sheria ya makosa ya kujamiiana (S3x.ual Offencea Act) yanatokana na mitandao,” alisema Jaji Mkuu wakati akijibu swali kuhusu sheria ya makosa ya mitandao.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga alisema kuitishwa kwa mkutano wa kupambana na rushwa nchini Uingereza ni mojawapo ya jitihada za Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzisha vuguvugu la uanaharakati wa mapambano dhidi ya rushwa.

 

“Kukosekana kwa utawala bora, changamoto za ugaidi, biashara za dawa za kulevya, biashara ya kusafirisha binadamu na uwepo wa rushwa na ufisadi ni baadhi ya mambo yaliyofanya dunia ibadilike. Haya mambo zamani yalikuwa hayana mahali pa kuzungumzwa, kwa hiyo vikao kama hivi vitasaidia kukabili tatizo hili,” alisema.

 

“Rushwa ni kama pweza mwenye vichwa vingi na mikia mingi. Waziri Mkuu David Cameron ameamua kuanzisha movement hii ili kutafuta njia za kukabili janga hili kubwa,” alisema.

 

"Sote tunatambua kuwa mataifa mengi yangependa kuwemo katika hii movement lakini ni faraja kuona kwamba Tanzania imo miongoni mwa waanzilishi na hii ni kwa sababu ya uongozi na ujasiri wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye kwa kweli ni game changer  (akimaanisha kuwa amebadili mwelekeo wa Taifa hili) kwani ana utashi wa kisiasa na ana ujasiri wa kukemea maovu,” alisema huku akishagiliwa

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola alisema vita ya rushwa nchini Tanzania ni endelevu na inafanyika kuitikia wito alioutoa Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la Tanzania Novemba 20, 2015.

 

Alisema wanatumia mbinu mbalimbali kupambana na rushwa lakini kubwa wanayoenda nayo hivi sasa ni kutoa elimu kwa watoto na vijana ili kuwabadilisha tabia na utamaduni uliojikita kwenye jamii.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAPILI, MEI 15, 2016.

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta