Thursday, October 6, 2016

Rais Magufuli Atangaza Kiama ....Ni cha Kuwanyang'anya Watu Wote Walioshindwa Kuendeleza Mashamba, Asisitiza Hatojali Hadhi ya Mtu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watu wote nchini wanaohodhi mashamba makubwa na kutoyaendeleza wafanye hivyo ndani ya mwezi mmoja kabla hayawanyang’aya mashamba hayo kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyonayo.

Akizungumza jana na wananchi mkoani Pwani wakati wa zoezi la kuzindua kiwanda cha kusindika matunda, Rais Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji wanaotaka kuja nchini kuwekeza wafanye hivyo kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha.

“Nataka watu wote wanaotaka kuja nchini kuwekeza waje, kwa kuwa ardhi ya kutosha tunayo na nawataka watu wote waliohodhi ardhi hata kama walikuwa viongozi huko nyuma nataka wayalime ndani ya mwezi mmoja na kama wasipofanya hivyo nitabatilisha hati zao za umiliki na kuwapa watu wengine ambao wapo tayari kuendeleza ardhi hiyo"Alisema Rais Dkt. John Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alisema baadhi ya wafanyabiashara wa sukari nchini wamekuwa siyo waaminifu kwa kuagiza sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani kutoka nje ya nchi sukari ambayo ikifika nchini huiweka kwenye mifuko na kuiuza kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani jambo linaloweza kuathiri afya za watumiaji.

“Tatizo la sukari liliingia baada ya kuanza kuifuatilia sukari ili sukari inayopakiwa kwa matumizi ya binadamu iwe hivyo ndipo wafanyabiashara wakaanza kuficha sukari, ndiyo maana ninataka wawekezaji waje hapa kuwekeza katika kilimo cha sukari ili sukari izalishwe hapa nchini” Alisema Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Rais Magufuli alikemea tabia ya watu kuficha pesa na wengine kuzigeuza katika mfumo wa dolla na kuzificha chini ya ardhi na kusisitiza wanaofanya hivyo mwisho wake watakuta pesa hizo zimeharibika huku akiwataka wazitumie kuwekeza katika viwanda.

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta