Sunday, May 15, 2016

Zifahamu Faida/Hasara za kurudiana na Mpenzi wako wa zamani

Kuna faida ya wapenzi kuachana na kurudiana? Vipi kuhusu hasara zake? Hiyo ndiyo mada yetu ya leo kama inavyojieleza. Bila shaka unawajua watu ambao walikuwa wakiishi pamoja kimapenzi, iwe ni ndoa, uchumba au uhusiano wa kawaida ambao wamewahi kutengana na baadaye wakarudiana, iwe ni mara moja au zaidi.
Yawezekana hata wewe ukawa miongoni mwa watu wa aina hiyo, kwamba uliwahi kutengana na mtu umpendaye lakini baadaye ukajikuta unarudiana naye na kuanzisha upya uhusiano.
Je, kuna faida na madhara gani kwa wapenzi kuachana kisha kuja kurudiana tena na kuanzisha upya uhusiano wa kimapenzi? Ukiwaona watu wanaoishi kwenye aina hii ya uhusiano wa kimapenzi unawachukuliaje?

NI JAMBO LA KAWAIDA KATIKA MAPENZI

Yawezekana aina hii ya uhusiano wa kuachana na kila mmoja akaendelea na maisha yake kisha baada ya muda mkarudiana tena, likaonekana jambo la ajabu au geni katika mila na desturi za Kiafrika lakini kwa taarifa yako, hili ni jambo la kawaida kabisa katika uhusiano wa kimapenzi duniani kote.
Takwimu zinaonesha kwamba asilimia kubwa ya wanandoa au watu ambao wapo kwenye uhusiano imara wa kimapenzi, wamewahi kupitia kipindi hiki kigumu cha kutengana na kurudiana, wengine wakifanya hivyo mara kadhaa.
Wapo baadhi ya watu ambao baada ya kutengana, hushindwa kukaa chini na kumaliza tofauti zao hata kama bado wanapendana kwa kuona jamii itawashangaa kuwaona wakiwa pamoja tena baada ya kuachana kwa kashfa na vurugu kubwa.
Kama na wewe ni miongoni mwa watu wa aina hii, narudia kukusisitiza kwamba hilo ni jambo la kawaida na linafanyika duniani kote.

MADHARA YAKE

Yapo madhara mengi yanayowakumba watu wanaoishi kwenye aina hii ya uhusiano. Inapotokea mmeachana na kila mmoja akaanzisha ukurasa mwingine wa mapenzi, lazima atakutana na mazingira tofauti kabisa na yale mliyozoea kuishi pamoja.
Endapo atakutana na mtu mwingine ambaye amekuzidi vitu vingi, hata ikitokea wakaachana na akarudi kwako, hawezi kukupenda kwa kiwango kile kama ilivyokuwa mwanzo kwa sababu tayari kuna vitu vipya vimeingia ndani ya kichwa chake na huo utakuwa ufa mwingine ambao hapo baadaye utasababisha muachane tena.
Upo ushahidi wa wapenzi ambao baada ya kutengana na watu waliokuwa wanawapenda mwanzo, walikutana na watu wengine wenye uwezo wa kuwaridhisha na kuwafurahisha faragha kuliko ilivyokuwa kwenye uhusiano uliovunjika. Inapotokea ukarudiana na mpenzi wa aina hii, ambaye tayari ameshauona ulimwengu mwingine wa kuridhishwa kimapenzi ambao kwako hakuwahi kuuona, kamwe hawezi kutulia na wewe. Hesabu maumivu.
Suala lingine ni maradhi. Katika dunia iliyochafuka kama hii tunayoishi, ni hatari kurudiana na mwenzi wako kwa sababu hujui baada ya kutengana na wewe alikuwa akitoka na nani. Ni rahisi kukuletea maradhi ya zinaa au Ukimwi hasa kama alikuwa anatoka na watu wasio sahihi. Unapaswa kuwa makini katika hili.
Kulipizana visasi ni tatizo lingine linaloweza kuwakumba watu wanaoishi kwenye uhusiano wa aina hii. Yawezekana wewe ndiye uliyemuumiza mwenzi wako wakati mnaachana, ukautesa moyo wake na kushindwa kumuonea huruma wakati akiteseka.
Inapotokea mmerudiana, wengi hubaki na vinyongo ndani ya mioyo yao na kwa sababu wewe ndiye uliyemuumiza na yeye atakutafutia sababu ya kulipa kisasi ili na wewe uhisi maumivu kama aliyoyahisi yeye wakati mnaachana.

FAIDA ZAKE

Narudia kusisitiza kwamba japokuwa wengi wanaona kama ni jambo la ajabu kurudiana na mtu uliyekuwa unampenda, ni jambo la kawaida kabisa na watu wengi wanafanya hivyo duniani kote.
Takwimu zikionesha kwamba wanandoa au wapenzi waliowahi kupitia kipindi cha kutengana kisha wakarudiana tena, wana nafasi kubwa ya kudumu kwenye uhusiano wao kwa kipindi kirefu zaidi.

Zifuatazo ni faida za kuachana na kurudiana.

TAYARI MNAJUANA: Mara nyingi unapoanzisha uhusiano mpya, unaweza kudhani kwamba unampenda sana mtu uliyenaye kwa sababu bado humfahamu kwa kina lakini ukishamjua kwa undani, hasa tabia zake, yale mapenzi uliyokuwa nayo huisha haraka kwa sababu ya upungufu utakaoubaini.
Unaporudiana na mwenzi wako, huanzi upya kwa sababu kama ni kumjua tayari unamjua na yeye anakujua, unaelewa udhaifu na uimara wake, hali kadhalika na yeye anakujua kwa hiyo mkiamua kuwa ‘serious’, kazi inakuwa nyepesi kuliko kuanza upya na mtu mwingine.
 
MMESHAKOMAA KIHISIA: Uamuzi wa kumrudia mtu aliyewahi kukuumiza, huhitajiujasiri mkubwa sana na ukiona umeweza kumsamehe na moyo wako bado unamhitaji, hiyo ni ishara ya ukomavu wa kihisia. Kama mkirudiana pamoja, hakuna tena jambo linaloweza kuwasumbua kwa sababu mmeshapitia milima na mabonde.
Kuna msemo mmoja maarufu kwamba huwezi kuona umuhimu wa kitu mpaka utakapokipoteza. Muda ambao mmeachana, kila mtu hupitia kipindi kigumu kihisia. Huu ndiyo muda ambao unaweza kupima kati ya mazuri na mabaya ya mwenzi wako, yapi yalikuwa mengi.
Ukiona moyo wako bado unamhitaji hata kama yapo aliyokukosea, tafsiri yake ni kwamba umeona umuhimu wake na utakapopata nafasi ya kurudiana naye utakuwa makini usimpoteze tena.
HISIA ZAKO ZIMETULIA: Inapotokea unakorofishana mara kwa mara na mwenzi wako, zile hisia tamu za mapenzi kati yenu hupotea kabisa na matokeo yake mnaishi kimazoea. Lakini inapotokea mmetengana na kila mmoja akaendeleana mambo yake, hisia hutulia na kurudi upya. Mnaporudiana kila mmoja anakuwa mpya kihisia hivyo mnakuwa na nafasi kubwa ya kudumu.
HAKUNA CHA KUWAYUMBISHA TENA: Wahenga wanasema nahodha mzuri wa meli hupimwa wakati bahari imechafuka. Ikiwa mmeshapitia kwenye machafuko makubwa yaliyosababisha mpaka mkaachana, wakati mwingine kwa vurugu kubwa, ni dhahiri kwamba kila mmoja ameshapata uzoefu.
Hata ikitokea mmekorofishana tena, hakuna atakayekuwa tayari kuona mnarudi kule mlikotoka hivyo mtamaliza vizuri tofauti zenu

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta