Wakati upelelezi wa tukio la watu saba wa familia moja kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana ukiendelea, mauaji mengine ya aina hiyo yametokea wilayani Sengerema.
Safari hii, mkazi wa Kijiji cha Bilulumo, Kata ya Kafunzo, James Mgambo (71) aliuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Kafunzo, Dotto Bulunda, mke wa Mgambo aliyetajwa kwa jjina la Nyangalo Masisa (65) alijeruhiwa katika tukio hilo na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema.
“Chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana na polisi wamefika kwa ajili ya uchunguzi,” alisema Bulunda.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bilulumo, Said Makelemo alisema mapanga mawili yanayoaminika kutumika yalikutwa eneo la tukio.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Lameck Kasabulilo alisema hawakusikia kelele za kuomba msaada.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Hakimu Elisha, mazishi ya Mgambo yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya ukoo yaliyopo kijijni hapo.
Mgaga Mkuu wa Hospitali Teule Wilaya ya Sengerema, Dk Mary Jose alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti, huku hali ya majeruhi ikiendelea vizuri.
Mkuu wa Wilaya Sengerema, Zainab Telack alisema tayari uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo umeanza na kuapa wahusika watasakwa na kutiwa mbaroni.
Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii