Sunday, May 22, 2016

Moto wa Ajabu wateketeza mjamzito, Mtoto na Bibi


Inauma sana! Familia ya Eliakunda Mbwambo imempoteza mke wake (Tatu Issa) mwenye umri wa miaka 50, binti yao aliyekuwa mjamzito (Rehema Mbwambo, 27) na mwanaye wa kwanza aitwaye Catherine Stewart (6). 

Hata hivyo, Eliakunda alinusurika na kukimbizwa hospitali akiwa hoi kutokana na ajali hiyo ya moto wa ajabu ambao haukufahamika chanzo chake nyumbani kwao Migombani, Minazi Mirefu, Kiwalani jijini Dar es Salaam. 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alidai huenda tukio hilo lina mambo ya kishirikina kwani nyumba hiyo haina umeme, wakati moto unatokea walikuwa wamezima kila kitu pia maajabu mengine ni kwamba moto umeanzia mlangoni lakini chumbani haukufika japokuwa baba aliyekuwa amelala huko kwa sasa yu hoi hospitali. 

“Huu moto ni wa miujiza kwani ukiangalia kwanza umeanzia mlangoni ambapo watu waliokuwa wamelala sebuleni yaani bibi, mtoto wake na mjukuu wake walikuwa wamelala hapo na kuungua vibaya huku baba ambaye alikuwa chumbani ambako moto unaonekana haukufika naye akiwa ameungua na sasa yu hoi hospitali jambo ambalo linatupa wakati mgumu kwamba inawezekana kuna mambo ya kishirikina,” kilisema chanzo hicho. 

Kwa upande wa jirani aliyejitambulisha kwa jina la mama Conso alisema wakati wa tukio hilo walisikia sauti zikiomba msaada kwamba wanakufa hivyo wakaamka na kukimbilia huko na kukuta moto ukiwa unawaka. 

“Ilikuwa ni saa nne usiku, Jumapili iliyopita ambapo nilisikia kelele zikiita mama Conso tunakufa tuokoe ndipo tukatoka na kukuta moto na tukaanza kufanya jitihada za kuuzima na kuwapigia fire ambao nao walikuja ambapo waliokolewa wakiwa wameshakata kauli lakini walienda kuaga dunia hospitali,” alisema mama Conso. 
 
Diwani wa kata hiyo ya Minazi Mirefu, Kassimu Mshamu akizungumza msibani hapo alisema kwamba amesikitishwa sana na tukio hilo kwani haijawahi kutokea hali kama hiyo, hivyo kupoteza watu watatu wa familia ni majonzi makubwa yasiyokuwa na mfano. 

“Nilipigiwa simu na wananchi wangu kwamba kuna tukio la moto na watu wamefariki ambapo niliungana nao, halijawahi kutokea tukio kama hili tena katika kata hii na limewaumiza watu wengi sana ndiyo maana unawaona wamefurika,” alisema diwani huyo. 

Akizungumza baba wa Catherine alisema ameumizwa sana na vifo hivyo kwani aliyekuwa anamuona ana nafuu ya kupona ni mwanaye lakini alifariki na kumuachia majonzi mazito. 

“Mimi na mama Catherine tuliachana miezi sita iliyopita hivyo baada ya kupata taarifa hizi nilifika na kwenda kuwahudumia hospitali lakini Mungu akawapenda zaidi, nakumbuka mwanangu alivyokuwa akilia na kuomba apelekwe hospitali anaumia huku akimuulizia mama yake na bibi. 

“Nilibaki namuuguza baba hospitali, alipata nafasi ya kuzungumza na kusema kwamba ule moto ulisababishwa na mtu lakini hakuongea zaidi mpaka sasa hali yake ni mbaya, nimekonda kwa sababu ya tukio hili jamani, inauma sana,” alisema baba Catherine.
 

CREDIT: GPL

Tupe Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

 

GOSSIPS Copyright © 2016 -- Template created by Mbatta